Friday, July 1, 2011

HISTORIA YA VICOBA

Home Page


Search

Photo Gallery

Home » Who We Are » History

Historia ya Fupi ya Shirika na Shughuli Zake
SEDIT ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa Februari 23, 2005 chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambalo makao makuu yake yapo Ilala Sharifu Shamba, kitalu namba 58. Shirika letu limekuwa likijihusisha na uanzishaji wa vikundi vya kuweka na kukopa katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia mfumo wa VICOBA (Village Community Banks) ambao ulianzishwa na shirika letu hapa nchini mwaka 2002 kutokana na mfumo wa MMD (Mata Masu Dubara) ambo umekuwa na mafanikio makubwa katika nchi nyingi za Africa kama Niger, Zimbabwe, Msumbiji, Uganda, na Eritria.
Shirika la SEDIT limekuwa likisaidiana na Mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje, Taasisi mbalimabi pamoja na Serikali hususani Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji Kitengo cha Kuondoa Umasikini katika kuanzisha na kusimamia mfumo huu wa VICOBA katika maeneo mbalimbali ya Tanzania. Miongoni mwa Taasisi na Mashirika hayo pamoja na maeneo waliyoanzisha mfumo huu katika mabano ni kama ifuatavyo: World Conference on Religion and Peace-WCRP/TZ (Kisarawe na Ukonga), miradi miwili ya kilimo inayoendeshwa na shirika la CARE Tanzania (Magu na Misungwi mkoani Mwanza), Mradi wa Hifadhi ya Milima ya Mahale (Kigoma Vijijini), Mradi wa Hifadhi ya Mto Ruaha Mkuu (Mbarali, mkoa wa Mbeya) pamoja na hifadhi za milima ya Udzungwa, Morogoro na Iringa katika wilaya ya Kilolo), mradi wa uhifadhi milima ya Mpanga/ Kipengele (Njombe na Makete), mradi wa uhifadhi maliasili za baharini na pwani (Rufiji, Mafia na Kilwa) inayosimamaiwa na shirika lisilo la kiserikali la WWF - Tanzania.

Pia miradi mingine ni pamoja na: mradi wa usimamizi wa barabara za wilaya na kuinua kipato cha wananchi unaoendeshwa katika Tarafa ya Matombo na ITECO Engineering kwa kusaidiana na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro (V), Mradi wa hifadhi ya misitu wa Ruvu Kusini na Kibaha unaoendeshwa na Shirika la CARE Tanzania, na mradi wa kuhifadhi ardhi na kuongeza kipato cha jamii (LAMP) unaoendeshwa katika wilaya ya Simanjiro, Kiteto, Babati (mkoa wa Manyara) na Singida vijijini unaofadhiliwa na shirika la kimataifa la SIDA, mradi wa kuhifadhi mazingira (FLORESTA) uliopo Marangu na maradi wa maendeleo ya wananchi wa kata ya Mletele (Songea). Miradi hii yote imeweza kuendesha mradi wa VICOBA kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia wataalamu kutoka SEDIT.

Kutokana na mafanikio haya, mwaka jana 2007, SEDIT iliamua kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa kwa kutumia mfumo wa VICOBA katika mkoa wa Dar es salaam Manispaa ya Ilala. ambapo katika awamu ya kwanza, (Januari hadi Desemba 2007), SEDIT imeweza kuanzisha jumla ya vikundi 10 vyenye wastani wa wanachama 25 kila kikundi katika katika maeneo yafuatayo: Kata ya Segerea mtaa wa Segerea (kikundi 1) na mtaa wa Kisukuru (vikundi 4), Kata ya Kinyerezi mtaa wa Kinyerezi (vikundi 5). Vikundi hivi 10 katika kipindi cha mwaka mmoja tu vimeweza kukusanya jumla ya Shs, 45,000,000/= kutoka kwa wanachama wake kwa njia ya kujiwekea akiba. Aidha wanachama wapatao 250 kutoka kwenye vikundi hivi wameweza kunufaika na mikopo ya biashara yenye thamani ya Shs. 55,000,000/= pamoja na mikopo ya kutatulia matatizo ya kijamii kwa wanachama na familia zao yenye thamani ya Shs. 5,000,000/=

Katika kipindi cha kuanzia Januari - Desemba, 2008, shirika la SEDIT limeazimia kuunda vikundi vya VICOBA 30 katika Manispaa ya Ilala hususani kutoka katika maeneo ya Tabata, Kinyerezi, Kisukuru, Buguruni, Vingunguti na Ilala na kupanua mradi kwenda katika maeneo mengine ya mkoa wa Dar es Salaam. Hivyo basi kwa sasa SEDIT inaendelea kupanua huduma zake za uanzishwaji wa vikundi katika maeneo hayo yaliyotajwa hapo juu.

Lengo kuu la mradi huu ni kusaidia jitihada za serikali za kuinua kipato cha wananchi na kuondoa umasikini. Katika kutekeleza azma hii shirika letu la SEDIT limekuwa likihamasisha wananchi kuunda vikundi vya VICOBA vyenye wanachama 25 hadi 30 kwa kila kikundi, kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa wanachama ili kuweza kusimamia miradi wanayoibuni.

Ili kupunguza tatizo la mitaji kwa wanachama, shirika la SEDIT limekuwa likisaidia katika kuanzisha na kusimamia mifuko ya vikundi ambayo huchangiwa na wanachama kwa njia ya Hisa ambapo wahisani mbalimbali huhamasishwa kusaidia jitihada za wanachama ili kutunisha mifuko hiyo. Mifuko hiyo hutumika kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanachama kwa ajili ya kuendesha biashara zao. Shirika letu pia limekuwa likisadia katika kutafiti na kuandaa mtandao wa masoko (market links) kwa wazalishaji wadogo wanaoshiriki katika mpango huu.

HISTORIA YA MFUMO WA VICOBA

MUUNDO, KANUNI NA TARATIBU ZA MFUMO WA KUWEKA NA KUKOPA VIJIJINI (VILLAGE COMMUNITY BANKS - VICOBA)

A) UTANGULIZI:
Mfumo wa Kuweka na Kukopa Vijijini (Village Community Banks - VICOBA) ni mpya hapa nchini kwetu, mfumo huu uliingizwa nchini na Shirika la CARE International, Tanzania mwaka 2000 na kuendeshwa kwa mara ya kwanza katika visiwa vya Ungunja na Pemba huko Zanzibar ambako unajulikana kwa jina la Jozani Savings and Credit Association - JOSACA

Mfumo wa VICOBA umeundwa kutokana na mfumo mama wa “Mata Masu Dubara - MMD’’ yaani Wanawake katika harakati za kutafuta maendeleo ulioundwa na Shirika la CARE International Niger mwaka 1991. Mradi huu ulianzishwa ili kusaidia kufanikisha jitihada za akinamama waishio vijijini za kupambana na umaskini kwa kujenga uwezo wao wa mitaji, kuwapatia elimu ya kibiashara na kuimarisha mshikamano na ushirikiano miongoni mwao.

Mradi wa MMD ulionyesha mafanikio makubwa sana katika mwaka wa kwanza ambapo Serikali ya Niger iliamua kushirikiana na Shirika la CARE Niger na kueneza mradi huu katika maeneo mengine mengi ya vijijini. Baada ya miaka mitatu ya uendeshaji mradi wa MMD uliweza kuhudumia wanachama wapatao 80,000. Kutokana mafanikio hayo mradi huo ulichangia kupanda kwa kipato cha wanachama wake kwa wastani wa asilimia hamsini (50%), na kwa hivyo kuwawezesha kumudu gharama za familia zao na kuchangia shughuli za maendeleo ya maeneo yao. Kwa ufupi mradi huu ulichangia kuongezeka kwa uzalishaji katika maeneo husika na kujenga ufahamu juu ya mbinu bora za maisha na kukuza ushirikiano miongoni mwa wananchi waishio vijijini.

Baada ya kuonyesha mafanikio mazuri viongozi wa shirika la CARE Zimbambwe, Msumbiji, na Uganda waliamua kuanzisha mfumo huu mpya wa kuweka na kukopa ili kuharakisha maendeleo ya watu na kuleta ufanisi mkubwa wa miradi yao. Uanzishwaji wa mfumo wa MMD katika nchi zilizotajwa hapo ju ulifanyika kama ifuatavyo: mwaka 1994 (Zimbambwe), 1996 (Msumbiji), na 1998 (West Nile - Uganda) ambapo sehemu hizo zote mfumo huu umeonyesha mafanikio mazuri, hii ikiwa ni pamoja na kuinua uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii vijijni, na kuchangia maendeleo ya kitaifa kwa kiwango kikubwa.

Katika nchi ya Msumbiji mfumo huu huitwa Ophavela na CARE Uganda huita JENGA yaani Joint Encouragement for New Gainful Activities.

Baada ya Shirika la CARE International, Tanzania kutambua mafanikio makubwa ya mfumo huu mwezi Oktoba 2000 lilituma maafisa wake kwenda kutembelea mradi wa JENGA nchini Uganda mmoja wapo akiwa ni Mr. George Sweveta mwenyekiti wa shirika la SEDIT kwa sasa, kujifunza mfumo huu ili uanzishwe katika miradi ya maendeleo inayoendeshwa na Shirika hilo hapa nchini hususani Visiwa vya Zanzibar, Magu na Misungwi mkoa wa Mwanza. Maafisa hao baada ya kurejea nchini walianzisha mradi majaribio wa kuweka na kukopa kwenye maeneo yanayozunguka msitu wa Jozani na Ghuba ya Chwaka huko Unguja, Zanzibar ambao unaitwa Jozani Savings and Credit Association (JOSACA) kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo ya hifadhi kuboresha kuboresha maisha yao kwa kuendesha miradi endelevu isiyoharibu mazingira.

Mradi wa Jozani, Zanzibar umeonyesha mafanikio makubwa sana kwa mwaka 2001 na 2002 kiasi cha kuwa mfano kwa miradi mingine ya mazingira na maendeleo ya jamii inavyoendeshwa na Shirika la CARE International kwa nchi zilizo kusini nwa jangwa la Sahara.

B) HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA MFUMO WA (VICOBA)
i) Uhamasishaji wa jamii na uundaji wa Vikundi vya Kuweka na Kukopa Vijijini (VICOBA) vinavyoendesha shughuli zao za kibenki wao wenyewe kwa njia ya kujitolea’
ii) Kusaidia vikundi katika kuaandaa vifaa vya kibenki na makala za kufundishia
iii) Kutoa mafunzo ya uongozi wa vikundi na mafunzo ya kuweka na kukopa katika maeneo yao
iv) Kutoa mafunzo ya biashara yanayolenga katika kuwawezesha wanachama kuweza kuchagua miradi mizuri ya kiuchumi, kuandaa mipango mizuri ya kuanzisha na kuendesha miradi yao ma mbinu za kusimamaia miradi hiyo kwa faidi.
v) Kutoa mafunzo ya teknolojia nyepesi kwa wazalishaji wadogo wadogo
vi) Kufanya utafiti wa masoko, kuandaa mikakati ya masoko kwa wazalishaji wadogo wadogo
vii) Kufanya tathmini ya uazalishaji na uendeshaji wa shughuli za kibenki, na kutoa ushauri kwa vikundi husika.
viii) Kusadia vikundi vya wazalishaji wadogo wadogo kubuni miradi endelevu ya kiuchumi, kusaidia kuratibu na kufuatilia usambazaji wa pembejeo na raslimali zingine za kibiashara.

C) MAFANIKIO YA MFUMO WA VICOBA NCHINI
Mradi wa Hifadhi ya Msitu wa Jozani na Kisiwa cha Misali, Zanzibar ni mfano mzuri sana wa kuigwa hapa nchini, ambapo hadi sasa wananchi wapatao 2144 (Vikundi 78) wamekwisha faidika na huduma hizo katika visiwa vya Unguja na Pemba

Kwa upande wa Tanzania Mfumo wa VICOBA hutumiwa na taasisi na Asasi mbalimbali za kimaendeleo ili kusaidia kuharakisha maendeleo ya jamii katika maeneo mabalimbali nchini na kuhifadhi mazingira. Miongoni mwa Taasisi na Mashirika hayo na maeneo waliyoanzisha mfumo huu katika mabano ni pamoja na: Mradi wa maendeleo wa wananchi wa kata ya Mletele (Kata ya Mletele, Songea), World Conference on Religion and Peace-WCRP/TZ (Wilaya ya Kisarawe), Shirika la Uhifadhi wa maliasili na mazingira - WCST (Hifadhi ya misitu ya Pugu na Kazimzumbwi, Kisarawe, Pwani), Miradi miwili ya kilimo inayoendeshwa ya Shirika la CARE Tanzania katika wilaya za Magu na Misungwi Mkoani Mwanza, Mradi wa Hifadhi wa Milima ya Mahale katika mkoa wa Kigoma, Mradi wa Hifadhi wa Mto Ruaha Mkuu katika wilay ya Mbarali katika Mkoa wa Mbeya pamoja na hifadhi za milima ya Udzungwa na Mpanga - Kipengele iliyoko mikoa ya Morogoro na Iringa inayosimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la WWF - Tanzania, Mradi wa usimamizi wa barabara za wilaya na kuinua kipato cha wananchi unaoendeshwa katika tarafa ya Matombo na kampuni ya ITECO Engineering kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, Mradi wa Hifadhi ya misitu wa Ruvu Kusini, Kibaha unaoendeshwa na Shirika la CARE Tanzania, na Mradi wa Hifadhi ya Ardhi na kuongeza kipato cha jamii (LAMP) unaoendeshwa katika wilaya za Simanjiro, Kiteto, Babati (Mkoa wa Manyara) na Singida Vijijini unaofadhiliwa na shirika la CIDA.

Kutokana na mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana kutokana na mfumo wa VICOBA, mashirika mengi tayari yameonyesha nia ya kutumia mfumo huu katika miradi yao ndani na nje ya nchi yetu.

Kukuubalika kwa mfumo huu nchini kunatokana na ufanisi wake katika kuwaletea maendeleo ya uhakika wananchi waishio vijijini ambao kwa miaka mingi wamehangaika kujikomboa na hali duni ya maisha yao kwa kutumia njia mbalimbali bila mafanikio. Isitoshe mfumo wa VICOBA huendesha shughuli za kuweka na kukopa kutokana na raslimali (hisa) zinazochangwa na wanachama wa vikund husika bila kutegemea sana msaada wa wafadhili na kusimam,iwa na wao wenyewe. Hali hii inawafanya waweze kuanzisha mradi haraka na bila matatizo makubwa na kuendesha shughuli zao kwa hali ya uelewano zaidi.

Idadi ya watanzania walikwisha jiunga na mfumo wa VICOBA hadi sasa inakadiriwa kuwa 25,542 sawa na vikundi 912 vyenye wastani wa wanachama 28 kila kimoja.

Wastani wa hisa zilizokusanywa na wanachama wote 25,542 inakadiliwa kufikia Tanzania shilingi 2,298,780,000 ambayo ni wastani wa thamani ya hisa sabini elfu za kila mwanachama, na kiwango cha jumla ya mikopo iliyo tolewa kwa vipindi tofauti kwa wanachama wote tangu mpango huu uanze mwaka 2001 inakadiriwa kufikia zaidi ya Tanzania shilingi 3,065,040,000 (Bilioni tatu, milioni sitini na tano na arobaini elfu tu) ambayo ni wastani wa mkopo wa shilingi laki moja na ishirini tu .

Vikundi vya Zanzibar vilivyoanzishwa mwaka 2001 vimefanikiwa kuweka hisa zenye dhamani ya kati ya Tsh. 5,000,000 na 50,000,000. Wanachama wa vikundi hivi wameweza kuboresha maisha ya familia zao kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi ya kudumu ya kiuchumi kama vile: kufungua mashamba ya miti, kununua vyombo vya usafiri, ufugaji wa nyuki, na kujenga nyumba bora za kuishi, kusomesha watoto wao, nk.

Pamoja na mafanikio haya makubwa vikund vy VICOBA Zanzibar pia vinachangia uboreshaji wa huduma za kijamii vijijni kama vile: ujenzi wa madarasa wa shule za msingi, ujenzi wa shule za awali, uingizaji wa umeme vijijini na kugharamia uingizaji wa maji ya bomba vijijni.

D) UIMARA WA MFUMO WA VICOBA DHIDI YA MIFUMO MINGINE YA KUWEKA NA KUKOPA NCHINI

1. Ni mfumo unaomilikiwa na kusimamiwa na wanachama wenyewe

2. Utendaji wa kazi zote hufanywa kwa njia ya kujitolea (bila kugharimu malipo yoyote)

3. Ni mfumo unaozingatia zaidi kujenga uwezo wa walengwa kimtaji na kiujuzi ili walengwa waweze kubuni miradi endelevu ya kifamilia na kuitumia vizuri mikopo wanayochukua kutoka kwenye benki za vikundi vyao

4. Ni mfumo rahisi katika kuendesha, unaotumia kumbukumbu rahisi zinazobuniwa kulingana na mazingira; kiwango cha ufahamu, mila na desturi za wanachama wa kikundi husika. Mfumo huu umeundawa kwa kuzingatia mifumo asilia wa uendeshaji wa shughuli za kuweka na kukopa wa kiafrika (UPATU)

5. Ni mfumo unaoweza kuanzisha mfuko wa kuweka na kukopa kwa kutumia hisa za wanachama wa kikundi na mapato mengine ya kikundi bila kutegemea sana kupatikana kwa msaada wa mitaji toka kwa wafadhili au kuchukua mikopo yenye masharti magumu.

6. Mfumo huu hujumuisha watu wa rika, jinsia na itikadi zote bila kubagua ili mradi wanao uwezo wa kutekeleza kikamilifu malengo na shughuli za kikundi chao

7. Ni mfumo unaoendeshwa kwa uwazi zaidi na ushirikishwaji wa wananchama wote wa kikundi kwa kutumia taratibu walizopanga wao wenyewe kwa kuzingatia mahtaji yao, mazingira na uwezo wao wa kutenda mambo.

8. Faida inayopatikana kutokana na shughuli za kikundi hugawanywa kwa wanachama.kwa kuzingatia mchango wa kila mmoja wao kwenye mfuk wa kikundi

9. Ni mfumo unaotoa fursa ya kuundwa kwa benki za kijamii za Wilaya, Tarafa au Kata kwa njia ya kuunganisha rasilimali za vikundi vya maeneo husika pamoja wawekezaji wengine binafsi

10. Mfumo huu unaruhusu kuanzishwa huduma nyingine za kijamii na kifedha ambazo zinasaidia katika kupunguza kasi ya ukali wa maisha, kuleta ufanisi wa kibiashara katika familia za wanachama na jamii kwa ujumla na hivyo kuweza kuleta maendeleo kamilifu katika jamii

11. Mfumo wa VICOBA ni mfumo shirikishi unaojengwa katika msingi ya upendo, ushirikiano na kuaminiana miongoni mwa wanachama wa kikundi. Kutokana na sharti hili muhimu, mfumo huu unachangia kwa kiasi kikubwa katika kurekebisha tabia za watu wenye tabia mbaya na wasiokubalika katika jamii na kuwafanya wawe raia wema, ili wakubalike kwenye vikundi na kudhaminiwa na wenzao

12. Mfumo huu unalenga katika kubadilisha taratibu mbaya (zisizoendelevu) za maisha na kuziwezesha familia hizo kujiewekea malengo maalum ya maisha na kuandaa na kuitekeleza mikakati ya kuyafikia malengo yao hatua kwa hatua. Hii ni pamoja na kuwa na matumizi mazuri ya fedha kutika familia, kujituma katika kufanya kazi.

13. Mfumo huu unaurahisi wa kupata mikopo ya masharti nafuu kijijini na husaidia kuwawezesha wakijiji (wanachama) kujiwekea hisa kila wiki katika benki yao katika eneo husika na kwa kiwango kidogo kulingana na uwezo wao pasipo na gharama yoyote..

E) MUUNDO NA TARATIBU ZA UENDESHAJI VIKUNDI VYA VICOBA

Muundo wa uongozi kikundi cha VICOBA huundwa na wajumbe tisa ambao huchaguliwa kidemokrasia kwa kuzingatia kazi za kila kiongozi na uwezo walionao. Miongoni mwa viongozi hawa ni: wajumbe watano wa Kamati Tendaji yaani Mwenyekiti, Katibu, Mweka Hazina, na wahesabuji fedha wawili. Kundi la pili ni la viongozi wa kikundi ni: washika funguo za sanduku la kikundi watatu na munza nidhamu wa kikundi.

Viongozi hawa huchaguliwa kidemokrasia na wanachama wote kwa kuzingatia sifa walizonazo katika kuongoza kikundi. Viongozi hawa hubaki madarakani kwa mzunguko mmoja ambapo sawa na miezi 9 - au zaidi

Mzunguko wa kikundi hufungwa kwa muda wa wiki moja (1) hadi tatu (3), mara nyingi hii, hufanywa wakati wa sherehe za kidini au za mwisho wa mwaka au wakati wa kazi nyingi za kilimo, ukame, au uhaba mkubwa wa chakula, maji nk.

Hisa zote zinazopatikana hugawanywa kwa wanachama pamoja na faida ili kusaidia kulipia gharama mbalimbali za familia kama vile kilimo, kununua chakula, nguo, ada za shule za watoto, na kugharamia sherehe na matumizi mengine mhimu ya familia.

Mzunguko hufungwa ili kutoa nafasi ya kutosha kwa wanachama kushiriki kikamilifu katika kutatua matatizo yanayozikabili familia zao kipindi hicho. Mzunguko mpya huanza mara ya muda uliopangwa kupunzika kwisha. Marekebisho mhimu ya sheria za kikundi, uongozi na taratibu za kuendesha mikutano ni mhimu kufanyika wakat wa kufunga mzunguko ili kuboresha ufanisi wa kikundi katika mzunguko unaofuata.

F) TARATIBU ZA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA VIKUNDI

Shughuli zote za vikundi vya VICOBA huendeshwa na wanavikundi wenyewe kwa njia ya kujitolea. Uzoefu unaonyesha kuwa wanavikundi huweza kuendesha vizuri shughuli zao baada ya kupatiwa mafunzo haya ya uongozi na usimamizi wa kazi za vikundi kutoka kwa wataalam wa mfumo wa VICOBA.

Kazi/wajibu wa wanakikundi ni:
- Kushiriki kwenye mikutano na mafunzo ya vikundi.
- Kuweka hisa za kila wiki.
- Kuendesha miradi ya kiuchumi.
- Kuchukua mikopo na kurejesha.
- Kuchangia mfuko wa jamii na bima ya mikopo.
- Kushiriki kikamilifu katika kuendesha miradi ya pamoja ya kikundi
Vikundi vya VICOBA huandaa mipango yao na kufanya maamuzi yote kwa njia ya vikao ; ambavyo ni mkutano wa kila wiki , Mkutano mkuu maalumu na mkutano mkuu wa kawaida wa mwaka.

G) HAKI YA KISHERIA YA VIKUNDI VYA VICOBA
Kwa sasa vikundi hivi huendesha shughuli zao chini ya sheria ya sekta isiyo rasmi na kuendesha shughuli zake chini ya uangalizi/ ulezi wa serikali za mitaa au halmashauri za miji na wilaya husika. Vikundi vinavyofadhiliwa na mashirika hulelewa na kupatiwa msaada wa kitaalam kupia mashirika yao pamoja na ofisi za serikali za maeneo yaonayohusika. Ili kuhakikisha taratibu zao zinafuatwa kikamilifu na wanachama wake ni mhimu vikundi kujitungia sheria ndogo ili kuthibiti ukiukaji wa taratibu zilizowekwa na kuhakikisha kwamba kila mmoja anawajibika ipasavyo.

H) MPANGO WA MAFUNZO WA VIKUNDI VYA VICOBA
Mafunzo ndio shughuli inayopewa kipaumbele zaidi katika mfumo huu wa VICOBA. Hii ni kwa sababu tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha kuwa kukosekana kwa ujuzi an mbinu za kibiashara ndio kiini cha matatizo yanayozorotosha jitihada za kuleta maendeleo endelevu nchini husuan kwa wananchi waishio vijijini.

I) AINA YA MAFUNZO

Mafunzo ya mfumo wa VICOBA yamegawanyika katika makundi makubwa matatu ambayo ni:-
(a) Mafunzo ya uongozi wa kikundi na uendeshaji wa shughuli za kuweka na kukopa
(b) Mafunzo ya mbinu za biashara ya “ kuchagua, kupanga na kusimamia mradi wa ki-uchumi”
(c) Mafunzo ya teknolojia rahisi za kuboresha ujuzi wa uzalishaji wa bidhaa za wana-kikundi kama vile ufugaji wa nyuki, (Bee keeping) kilimo bora cha mbogamboga kazi za mikono n.k

Mafunzo haya hutolewa kabla ya wanachama wa kikundi kuchukua mkopo. Lengo la mafunzo haya ni kuwaandaa wana-kikundi kiujuzi na kuwawezesha, kubuni, miradi mizuri ya kiuchumi na kuandaa mipango ya namna nzuri ya kuendesha na kusimamia biashara hizo.

Mafunzo ya Kuweka na Kukopa na yale ya mbinu za biashara hutolewa kwa kipindi 12 kila wiki wanakikundi hufundishwa kipindi kimoja. Wakati huu wa mafunzo pia huweka akiba zao kwa njjia ya hisa ili kutunisha mfuko wao ambao baadaye hutumika kwa kukopeshana.

Mafunzo ya teknolojia rahisi hutolewa kwa wana-kikundi wanaoiendesha miradi ya uzalishaji bidhaa mbalimbali kama vile kazi za mikono, ufugaji, kilimo cha mbogamboga na shughuli zingine zinazohitaji ubunifu na mafunzo maalum. Mafunzo haya hutolewa ili kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa

Uchangiaji wa gharama za mafunzo
Kwa kawaida wanachama wa VICOBA hufundishwa mafunzo wanayotaka wao wenyewe. Vikundi vimeanzishiwa mfuko wa mafunzo ambao kila mwanachama huchangia kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kuchangia gharama za mafunzo haya.

Kutokana na uwezo mdogo wa wanvikundi, wafadhili mbalimbali ikiwemo Serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakijitokeza kuchangia gharama ya mafunzo haya. Mfano Mashirika ya CARE Tanzania, WCRP, WCST, WWF, Ofisi ya Makamu wa Rais, WWF Tanzania, ITECO Engineering, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Uropean Union, shirika lisilo la kiserikali la LAMP, Orgut nk

J) TARATIBU ZA UWEKAJI HISA ZA WANACHAMA
Kulingana sheria mama za mfumo huu wa VICOBA, mwanachama anatakiwa kuweka hisa 1-3 kila wiki. Kiwango cha hisa huamuliwa na wanakikundi wenyewe. Hata hivyo, kulingana na thamani ya fedha yetu kiwango cha chini kinachoweza kumnufaisha mwanachama kwa sasa ni shilingi mia tano (500). Mwanachama anaruhusiwa kuweka hisa moja, mbili hadi tatu kila wiki ili kutunisha mfuko.

Matumizi ya Hisa ya mwanachama

Hisa ni muhimu zana kwa mwanachma kwa sababu zifuatazo:
(i) Ni akiba ya mwanachama ambayo huichukua mwishoni mwa mzunguko pamoja na faida au wakati mwingine wowote apatapo matatizo kulingana sheria za kikundi chao. Kwa kawaida hisa zinazochukuliwa katikati ya mzunguko hutolewa bila faida
(ii) Hisa hutumika kama kigezo ch akujua kiwango cha mkopo ambacho mwanachama wa kikundi anaweza kuomba kutoka kwenye benki yao. Mumo wa VICOBA unamruhusu mwanachama kuchukua mkopo hadi mara tatu ya hisa alizoweka. Hata hivyo, uamuzi wa kupatiwa mkopo huo utazingatia matumizi na uhakika wa mwanachama kumudu kurejesha kwa wakati unaotakiwa.
(iii) Hisa hutumika kama dhamana ya mkopo unaotolewa kwa mwanachama wa kikundi kidogo cha watu watano (5). Dhamana ya awali ni ya mkopaji mwenyewe (Primary Guarantor) na dhamana ya pili ni ya wanachama wenzake wane (4) wa kikundi kidogo (Secondary Guarantors)

Hii inamaanisha kuwa ili kuhakikisha kuwa mikopo yote inayotolewa kwa wanachama 5 wa kikundi kidogo inadhaminiwa kikamilifu mambo yafuatayo yanatakiwa kuzingatiwa:
(a) Wanachama wa kikundi kidogo wasiruhusiwe kuchukua mkopo wakati mmoja. Tofauti ya mwezi mmoja hadi miezi miwilli ni kipindi kizuri kwa wastani wa watu wawili wawili kila awamu
(b) Kunatakiwa pawepo na makubaliano maalum baina ya mwanachama anayekopa na wale wanaomdhamini juu ya hatua zinazoweza kuchukuliwa na wadhamini endepo mdhaminiwa hatatimiza wajibu wa kulipa deni lake kwa uzembe
(c) Mwanachama anyekopa kutoka kwenye benki ya kikundi anatakiwa kuchangia mfuko wa bima ya majanga itakayokubaliwa na kikundi kwa mfano kufariki kwa mkopaji, kuugua kwa muda mrefu na kupoteza uwezo wa kufanya kazi/ kulemaa kwa mkopaji kuunguliwa au kuibiwa mali za biashara ya mkopaji, ukame, nk

Taratibu za utoaji na urejeshaji wa mikopo

Mikopo inayotolewa kwa wanachama wa VICOBA unatakiwa kurejeshwa na nyongeza (Interest) ndogo ambayo hutumika kwa kutunisha mfuko wa kikundi. Nyongeza hii hugawanywa kma faida kwa wanachama kwa kuzingatia kiwango cha hisa alizoweka kila mmoja. Mikopo ya mwanzo ambayo kwa kawaida huwa midogo kuliko mikopo inayofuata hutakiwa kulipwa kwa kipindi cha miezi 3 – 6. Lengo ni kumwezesha mkopaji aweze kulipa haraka na kuchukua mkopo mkubwa pale hisa zake zinavyopanda ambao utamwezesha kumudu kuanzisha na kuendesha biashara madhubuti zaidi

Mfumo wa VICOBA unamtaka mkopaji kurejesha mkopo aliokopa mwishoni mwa kipindi cha mkopo wake kwa awamu moja. Mkopaji anatakiwa kulipa sehemu ya nyongeza inayoiva kila ifikapo wiki ya mwisho ya mwezi. Sehemu ya mwisho hulipwa pamoja na mkopo

Mfano:
Endapo mwanachama atakapokopeshwa shilingi 100, 000.00 kwa nyongeza ya 10% (10,000.00) kwa kipindi cha miezi mitatu atarejesha kama ifuatavyo:-

Mwezi wa 1 Mwezi wa 2 Mwezi wa 3 Jumla
3,400 3,300 3,300 100,000 110,000

Endapo mkopo wa thamani hiyo hiyo (Shilingi 100, 000.00) utarejeshwa kwa kipindi cha miezi sita kwa gharama (nyongeza) ya asilimia ishilini 20% (20,000.00), marejesho yatakuwa kama ifuatavyo:-

Mwezi wa 1 Mwezi wa 2 Mwezi
wa 3 Mwezi
wa 4 Mwezi wa 5 Mwezi
wa 6 Jumla
3,400 3,400 3,300 3,300 3,300 3,300 100,000 120,000

Kwa kawaida mwanachama anayemaliza kurejesha mkopo wake vizuri anaruhhusiwa kuomba mkopo mwingine mara moja ili kufidia pengo la mtaji katika bishara yake.

Ufuatiliaji na Uthibiti wa shughuli za vikundi vya VICOBA

Makatibu wa vikundi vya VICOBA wanatakiwa kufuatilia mwenendo wa vikundi vyao na kuandaa taarifa za kila mwezi, miezi mitatu na taarifa za kila mwaka ambazo hujadiliwa na kupitishwa na mikutano mikuu ya vikundi vyao.

Afisa (Mkufunzi) anatakiwa kutoa maelekezo na msaada wa kiufundi pale inapobidi na kuwajulisha wafadhali wa vikundi na wadau wengine juu ya maendeleo ya vikundi kadiri inavyotakiwa.

No comments:

Post a Comment